Rweikiza, Karamagi waigawa CCM Bukoba Vijijini
Vumbi la kuwania ubunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, limeanza kutimka hata kabla ya filimbi kupulizwa baada ya wanaotajwa kuwania nafasi hiyo pamoja na wapambe wao kuanza maandalizi kwa kasi.
Kama ilivyo kwa wanaotajwa kutaka kuwania kiti cha Rais katika uchaguzi mkuu ujao, Jimbo la Bukoba Vijijini linaweza kutumika kama kielelezo cha harakati zinazoendelea takribani katika majimbo yote nchini.
Harakati zilizopo zinakwenda sambamba na uundaji wa timu za ushindi na huu ni wakati wa wanasiasa na wanachama kufanya uasi na usaliti na baada ya vumbi la uchaguzi mkuu kutua wanaweza kukaa na kupatana.
Nyuma ya mbunge aliyepo sasa, Jasson Rweikiza, kuna kivuli cha Nazir Karamagi ambaye ziara zake za mara kwa mara jimboni humo za kuimarisha chama na kusaidia miradi mbalimbali zinahusishwa na harakati za kutaka kugombea.
Mbunge huyo wa zamani, alibwagwa na Rweikiza katika kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na tangu wakati huo vigogo hao wawili wanaendesha mapambano tofauti ya kujiimarisha.
Mgawanyiko
Harakati za wanasiasa hao pia zimewagawa viongozi wa chama ngazi ya wilaya. Ni kutokana na mgawanyiko huo, kila kiongozi anashiriki ziara za mwanasiasa anayemuunga mkono na kususia ziara zinazoandaliwa na upande wa pili.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu uliopita, Nazir Karamagi hakupotea kabisa katika siasa za jimbo hilo. Kuwepo kwake kulimuwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Halmashuri Kuu (Nec) nafasi anayoitumia kwenye jukwaa la siasa kwenye jimbo hilo.Hivi karibuni Nazir Karamagi alifanya ziara katika kata zote na kutoa bendera za CCM na kuchangia ujenzi wa maabara.
Siku chache baadaye, Rweikiza alionekana kufuta nyayo alizokanyaga Karamagi kwa kupita maeneo yaleyale na kutoa mchango mara mbili zaidi.
Ziara ya Rweikiza ilisisimua wananchi hata katika majimbo jirani, baada ya kubadili njia ya mapambano na katika hatua hii, alitua kila kata akitumia chopa ‘helkopta’ suala lililoacha gumzo mpaka sasa.
Mwenyekiti akoleza pambano
Katikati ya pambano hili, yupo Mwenyekiti wa chama hicho wa Wilaya ya Bukoba Vijijini, Novatus Nkwama ambaye kauli na vitendo vyake vinampambanua kama mwamuzi ambaye tayari analo jina la mshindi mfukoni mwake.
Maoni
Chapisha Maoni