Massaburi ampigia chapuo Pinda urais 2015

Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat), Dk Didas Massaburi amempigia ‘debe’ Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba, ndiye anayehitajika kupewa ridhaa ya kuongoza nchi katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Dk Massaburi alisema hayo jana wakati wa kuzindua mchakato wa maadhimisho ya miaka 30 ya Alat na serikali za mitaa, kuwa Pinda ni kiongozi mwenye sifa zinazohitajika ndani ya jumuiya hiyo. Alizitaja baadhi ya sifa hizo kuwa ni pamoja na upole, mtu asiye dikteta, awe makini na asiyefanya uamuzi bila kupata ushauri.
“Kama Waziri Mkuu Pinda anazo sifa hizo zinazohitajika kwa Alat kwa nini nisiseme ukweli? ...ee kama kuna wengine wana sifa tunazohitaji basi tutachambua hapo baadaye, lakini ifahamike kwamba sina masilahi mengine na urais kwani kama ingekuwa vinginevyo basi ningetangaza nia mwenyewe,” alisema Dk Massaburi.
Aidha, Dk Massaburi ambaye pia ni Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam alisema kwa kipindi kirefu amekuwa na matarajio ya kuona rais ajaye anatekeleza na kusimamia maslahi ya jumuiya yao. Pia aliwataka mameya wote nchini kumuunga mkono rais mwenye sifa na vigezo hivyo.
Aliongeza kuwa jumuiya hiyo kwa sasa inapigania kuona maendeleo yanajengwa kuanzia ngazi za mitaa ambako ni msingi wa ukuaji uchumi wa taifa lolote lile duniani.
“Kujenga fly over (barabara za juu) au za lami mikoani haiwezi kumsaidia moja kwa moja mwanakijiji ambaye anahitaji kuboreshewa barabara za ndani, unakuta mtu anafunza miguuni kule Kibondo lakini barabara imepita ya lami, sasa unajiuliza inamsaidiaje,” alisema Dk Massaburi na kuongeza:
Kuhusu sakata la escrow
Akitoa maoni yake kuhusu sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Dk Massaburi alisema suala hilo limepotoshwa na baadhi ya wabunge kuwa fedha hizo ni za umma, jambo ambalo siyo sahihi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kutokana na uzoefu wake katika masuala ya hisa za kampuni, amegundua kuwa sakata ta escrow linachochewa na makundi mawili.
“Kundi la kwanza ni wapotoshaji wakiwamo wabunge, wachumi ambao walikuwa wakisambaza upotoshaji huo kwa masilahi yao binafsi...mtu mwingine anaweza kusema ninatetea labda nimepata mgao, hapana...ila ukweli unatakiwa uelezwe wazi.”
Dk Massaburi alitaja kundi lingine aliloliita la fisi ambalo lina idadi kubwa ya wapambe waliokuwa na njaa ya kupata mgao huo.
Alisema katika hakuna kiongozi anayetakiwa kuwajibishwa kutokana na ukweli kwamba, Kampuni ya Mechmar ndiyo iliyosababisha kuwapo kwa tatizo hilo.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao