Namna VVU inavyoongeza kasi ya saratani kumuandama binadamu

Wakati dunia ikiwa imeadhimisha Siku ya Ukimwi wiki hii, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara inayokabiliwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani, huku wengi wakibainika kuathirika na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Wataalamu wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wanasema kuna uhusiano kati ya VVU na saratani.
Hata hivyo, wanasema si kila mwenye saratani ana VVU, lakini kuwapo kwa ugonjwa huo, unaonea zaidi kwa njia ya ngono, kunachochea maradhi hayo.
Maradhi ya saratani yanayoambatana na VVU ni pamoja na shingo ya kizazi na ngozi yanayojulikana kwa kitaalamu kama Kaposis Sarcoma.
Takwimu za saratani zinaonyesha kuwa Tanzania kila mwaka inagundua wagonjwa wapya 21,180 na zaidi ya 16,000 hufarika kila mwaka kutokana na ugonjwa huo. Daktari bingwa wa saratani kutoka Taasisi ya Ocean Road, Dk Harrison Chuwa anasema ongezeko la watu waliogundulika na saratani wengi wao wamekutwa na virusi vya ukimwi, hivyo kufanya VVU kuwa chanzo cha ongezeko la ugonjwa huu tishio.
“Mara nyingi saratani inalandana na maambukizi ya virusi vya ukimwi na haina maana kwamba wote wenye magonjwa haya wana VVU.
Anasema licha ya uwapo wa ARV, wengi wamekuwa wakishambuliwa na saratani. Hata hivyo, awali wanawake waliokoma hedhi ndiyo ambao walionekana zaidi kupatwa na saratani ya shingo ya kizazi, lakini kwa hivi sasa imekuwa tofauti.
“Tunapokea wanawake kuanzia miaka 20 mpaka 40 kwa wingi wenye maambukizi ya saratani ya shingo ya kizazi, lakini ukichunguza wengi wao wana maambukizi haya, hata walio na matezi wengi wana VVU,” anasema Dk Chuwa.
Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa katika Kitengo cha Patholojia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Henry Mwakyoma anasema hata hivyo wanaobainika kuwa saratani ya ngozi baada ya uchunguzi wengine wana VVU.
Anasema VVU inachangia kuwapo kwa wagonjwa wengi wa saratani hasa kwa kueneza viruzi vya HPV.
“Hata hivyo Muhimbili tumekuwa tukipokea watu ambao wamechelewa sana na tukishawafanyia uchunguzi tunabaini kwamba wana saratani,” anasema Dk Mwakyoma.
“Human papilloma virus (HPV) Squamos cell carcinoma kirusi namba 16 na Adenocarcinoma namba 18, ni kati ya virusi 40 vinavyosababisha saratani ya tumbo la uzazi na vyenyewe vinachangia tatizo la saratani ya shingo ya kizazi kwa asilimia 70, huku asilimia 80 ya wagonjwa wakiwa wameambukizwa kwa ngono na wengine wakiwa tayari na VVU.”

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao