Karibu Profesa Assad, weledi ndiyo siri pekee
Rais Jakaya Kikwete amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, uteuzi wa Profesa Assad ulianza Novemba 5. Uteuzi wa profesa huyo mshiriki aliyekuwa katika Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni wa kuziba pengo lililoachwa na Ludovick Utouh ambaye amestaafu kazi hiyo kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.
Tunaungana na wananchi wengine kumpongeza Profesa Assad kwa uteuzi huo tukiamini kwamba weledi wake katika fani hiyo na misingi mizuri iliyowekwa na mtangulizi wake, vitamrahisishia kazi zake katika taasisi hiyo nyeti ambayo imejijengea heshima kubwa ndani na hata nje ya nchi kutokana na jinsi inavyotimiza majukumu yake.
Katika kipindi chake cha uongozi, Utouh aliifanya taasisi hiyo kuwa maarufu hususan baada ya Rais Kikwete kuridhia ripoti za CAG kupitia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, hatua ambayo imeifanya ofisi hiyo kuwa tegemeo kubwa katika kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha na mali ya umma.
Chini ya Utouh, tulishuhudia ukaguzi wa kina uliogusa karibu kila sekta ya umma, jukumu ambalo, kwa kupitia kamati za Bunge na Bunge lenyewe lilichangia kwa kiwango kikubwa nidhamu ya matumizi.
Tulishuhudia hatua mbalimbali za kinidhamu zikichukuliwa dhidi ya watendaji waandamizi wa Serikali na kisiasa katika kipindi cha Utouh kwa wale waliokiuka sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za umma. Mfano mzuri ni ripoti yake ya mwaka 2012 ambayo iliwang’oa mawaziri sita kati ya wanane ambao wizara zao zilionekana kugubikwa na ufisadi wa fedha za umma.
Ripoti hiyo ilimlazimu Rais Kikwete kupangua baraza lake la mawaziri na kuwang’oa, Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na William Ngeleja (Nishati na Madini).
Baada ya kutoka kwa ripoti hiyo, Utouh alikaririwa na vyombo vya habari akiwatahadharisha mawaziri walioteuliwa kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wengine kwamba wanapaswa kutimiza majukumu yao kikamilifu kwa kuwa ripoti zake hivi sasa zina nguvu ya kusimamia uwajibikaji, hivyo wanapaswa kusimamia vyema wizara zao kuzuia ubadhirifu wa fedha za umma.
Aliwaambia kuwa tangu wakati huo hadi mwaka 2015, kulikuwa na ripoti nyingine tatu, hivyo wachukue tahadhari kwa kuwa wao ndiyo wasimamizi wakuu wa shughuli za wizara na kwamba kilichokuwa kimetokea bungeni wakati ule hadi mawaziri kuwajibishwa, kilithibitisha kuwa sasa kutakuwa na uwajibikaji mkubwa utakaosababishwa na ripoti zake kama watendaji wasipofuata taratibu za Serikali. Kauli ya CAG huyo mstaafu imethibitishwa na kilichotokea katika Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu taarifa ya ukaguzi maalumu wa miamala iliyofanyika katika Akaunti ya Tegeta Escrow pamoja na umiliki wa Kampuni ya IPTL.
Siku za mawaziri waliotajwa kwenye sakata hilo lililohusu uchotwaji wa Sh306 bilioni pamoja na Mwanasheria Mkuu, zinahesabika baada ya Bunge kuishauri Serikali iwawajibishe. Tumejaribu kurejea haya kuonyesha dhima inayomkabili Profesa Assad katika ofisi yake mpya tukimtarajia kwamba ataanzia pale mwenzake alipoishia na kufanya makubwa zaidi.
Tunaamini kuwa atafanya kazi yake kwa weledi na kwa kuzingatia maadili bila kukubali shinikizo la viongozi serikalini au wanasiasa.
Maoni
Chapisha Maoni