Peshmerga wawajeresha nyuma IS

Operesheni ya siku mbili ya kijeshi ya wapiganaji wa Peshmerga katika jimbo la Kurdistan imefanikiwa kufungua njia kuelekea Mlima Sinjar, uliokuwa umezingirwa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.

Mafanikio haya ni muhimu sana katika mapambano ya kuuchukuwa mji wa Sinjar, ulio chini ya mlima wenye jina hilo hilo, ambao ulichukuliwa na IS tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu. Mkuu wa Baraza la Usalama la Mkoa wa Kurdistan, Masrur Barzani, amesema vikosi vya Kikurdi vilisonga mbele jioni ya jana kuelekea kwenye mlima huo.
"Leo tumekamilisha operesheni ambayo tuliianza jana, na ambayo inasimamiwa na mwenyewe Rais Masoud Barzani, ikihusisha eneo zima kutoka Zumar hadi Mlima Sinjar, kulikomboa eneo kubwa la Kurdistan, na pia kuwaokoa watu wa jamii ya Yazidi waliokwama mlimani. Ilikuwa operesheni kubwa na tunashukuru imefanikiwa," amesema kiongozi huyo.
Maelfu ya Wayazidi walikuwa wamekwama kwenye mlima huo mwanzoni mwa mwezi Agosti, wakati wapiganaji wa IS walipoichukua miji hiyo ya Sinjar na Zumar, na hivyo kuchochea wimbi kubwa la uhamaji.
Licha ya kwamba wengi wao waliondoshwa kwa njia ya anga au kusindikizwa na vikosi vya usalama kupitia Syria na kisha kurudi Iraq kujihifadhi kwenye jimbo la Kurdistan, lenye mamlaka yake ya ndani, lakini wengine wengi walikuja baadaye na kubakia wamekwama mlimani.Vijiji ambavyo vimechukuliwa hivi karibuni na vikosi vya Peshmerga vinaonesha ishara za mapigano makubwa, huku majengo mengi yakiwa yameharibiwa vibaya kwa mashambulizi ya anga ya Marekani. Mkuu wa operesheni ya Marekani, Luteni Jenerali James Terry, amesema eneo lililochukuliwa na peshmerga lina ukubwa wa kilomita za mraba 100.
Katika hatua nyengine, Marekani inasema operesheni yake ya kijeshi nchini Iraq na Syria imewauwa viongozi kadhaa wa IS, katika siku za hivi karibuni. Msemaji wa jeshi, Admirali John Kirby, amesema wanaamini kuwa IS imepoteza viongozi wake muhimu wa ngazi za juu na kati, miongoni mwao ni Haji Mutazz, naibu wa kiongozi mkuu wa IS, Abu Bakr al-Baghdadi.
Wengine ni Abdulbasit, ambaye alikuwa akishughulikia wapiganaji wa kigeni, na Radhwin Talib, ambaye alikuwa msimamizi wa IS kwenye mji wa Mosul. Jarida la Wall Street liliripoti hapo awali kwamba vikosi vya Marekani vilikuwa vimewalenga viongozi kadhaa muhimu wa IS, likimnukuu Mkuu wa Majeshi, Jenerali Martin Dempsey.
Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya IS mwezi Agosti mwaka huu, ambayo sasa yanazijumuisha nchi kadhaa washirika, ndani na nje ya Ghuba na Mashariki ya Kati.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao