Mbeya yakwama tena kufikia BRN katika elimu
Mbeya. Mkoa wa Mbeya kwa mara ya pili umeshindwa kufikia asilimia 60 ya ufaulu wa darasa la saba iliyopangwa na Serikali katika kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) baada ya kufaulisha kwa asilimia 46.4 wanafunzi wa darasa la saba mwaka huu.
Mwaka jana mkoa huu ulifaulisha asilimia 44 na kushika nafasi ya 16 kitaifa jambo ambalo Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwaagiza viongozi kuhakikisha wanarudisha hesima ya mkoa.
Katibu Tawala Msaidizi (Elimu), Regimius Ntyana aliwaambia wajumbe wa Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) kwamba mwaka 2008 , wanafunzi 75,733 waliandikishwa darasa la kwanza, lakini walioacha na kutofanya mitihani ya kumaliza msingi wanafunzi 14,061.
Kuhusu utoro wa wanafunzi kwa jumla mwaka huu, alisema wanafunzi 10,900 wakiwamo wa 6,400 wa sekondari wameacha shule mkoani Mbeya na kwa sasa wanatafutwa mahali popote walipo.
Akifafanua kuwa sekondari watoro walikuwa 4,418 wakati waliofariki dunia ni 44 na waliopata mimba ni 69. Akijadili tatizo hilo, Mbunge wa Songwe Philip Mlugo, aliwasihi viongozi kushirikiana na wananchi kuhakikisha wanafunzi walioacha shule wanarudi madarasani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deosdatus Kinawiro kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mbeya, alisema Tangu Januari hadi Septemba Serikali imefanikiwa kuwarudisha shuleni wanafunzi 138 tu wakiwamo 44 wa shule za msingi.
Maoni
Chapisha Maoni