Mawaziri wakutana Brussels kujadili kitisho cha IS
Mawaziri kutoka takriban nchi sitini walio katika muungano wa kupambana kijeshi dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la Dola la Kiislamu IS wanakutana hii leo kwa mkutano wa ngazi ya juu mjini Brussels
Kerry, waziri mkuu wa Iraq Haider al Abadi na mawaziri wa mambo ya nje kutoka bara Ulaya, nchi za kiarabu na nchi nyingine wanakutana katika makao makuu ya Jumuiya ya kujihami ya NATO kutathimini hatua zilizopigwa na mikakati bora ya kukabaliana na wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu IS.
Viongozi hao pia watajadili jinsi ya kuzuia kusafiri kwa wapiganaji wa kigeni kuelekea Syria na Iraq kujiunga na IS kundi ambalo limewavutia mamia ya vijana kutoka nchi za magharibi.
Kundi la IS limezua hofu kubwa kote duniani kutokana na kampeini yake ya kikatili ya kuyateka maeneo makubwa nchini Iraq na Syria, kuwaua raia wa nchi hizo na wafanyakazi wa kigeni waliotekwa na kukatwa vichwa.
Nchi sitini zinashiriki
Mnamo mwezi Agosti, Marekani ilianzisha mashambulizi ya kwanza ya angani dhidi ya IS nchini Iraq na mwishoni mwa Septemba kwa usaidizi wa nchi kadhaa washirika walianzisha kampeini ya kijeshi ya mashambulizi ya angani nchini Syria.
Saudi Arabia, umoja wa falme za kiarabu, Jordan na Bahrain zinashiriki katika mashambulizi ya angani nchini Syria huku Austarlia, Ubelgiji, Canada, Denmark, Ufaransa na Uholanzi zikishiriki katika mashambulizi ya angani Iraq.
Marekani hivi karibuni imethibitisha kuwa Iran ambayo sio mshirika wake kufikia sasa katika kampeini hiyo ilifanya mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambo wa IS mashariki mwa Iraq.
Nchi nyingine ambazo zimejumuishwa katika muungano huo wa nchi sitini unaoongozwa na Marekani zinatoa usadizi wa kiufundi kama kutoa taarifa za kijasusi.
Mipango makuhusi kulikata makali IS
Maafisa wamesema mawaziri hao wataangazia pia jinsi ya kukatiza vyanzo vinavyoipa IS fedha za kuendesha operesheni zake na namna ya kutoa msaada wa kibinadamu kwa waliotoroka makaazi yao nchini Syria na Iraq.
NATO imesema imeruhusu mkutano huo kufanyika katika makao yake kwasababu wengi wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo walikuwa wanakutana hapo jana lakini haishiriki katika kampeni hiyo ya kijeshi dhidi ya IS.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ambaye anahudhuria mkutano huo amesema umoja huo unaweza kutoa msaada wa kibinadamu na wa kisiasa kupambana na IS na kusisitiza kuna haja ya kutozungumzia masuala ya kidini katika mkutano huo kwani kundi la Dola la kiislamu haliwezi kuhusishwa na Uislamu kwani ni kundi la kigaidi lisilofuata misingi ya Uislamu.
Mwandishi:Caro Robi/Dpa/Afp
Mhariri: Elizabeth Shoo
Maoni
Chapisha Maoni