Chiza kufunguka sakata la uingizwaji sukari leo

SIKU moja baada ya Tanzania Daima kuripoti kuhusu sakata la sukari inayoozea katika maghala ya kiwanda cha Kilombero mkoani Morogoro, hatimaye Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhandisi Christopher Chiza, amesema leo atalitolea ufafanuzi suala hilo kwa kina.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima, Chiza alisema suala la uagizaji sukari haliihusu Wizara yake tu, bali ni suala mtambuka.
Kutokana na hivyo, alisema katika mkutano huo ataweza kufafanua kile kinachoendelea katika mgogoro huo, ambako waagizaji sukari na wazalishaji wa viwandani wamekuwa wakituhumiana kuhusu biashara hiyo.
“Kwangu wote hawa nawaita ni wafanyabiashara na waandishi mnapaswa kuelewa hivyo, nimesoma mengi kuhusu sakata hilo na nimekuwa nikipigiwa simu na waandishi mbalimbali, hivyo nimeona ni vema nikaitisha mkutano ili kuwaeleza kwa pamoja kinachoendelea,” alisema Waziri Chiza.
Pia, Tanzania Daima ilifanya juhudi za kuwatafuta waagizaji wa sukari wanaotuhumiwa kuhujumu biashara hiyo, ambako Mwenyekiti wa Kampuni ya Mohamed Enterprises, Gulam Dewji, alisema anashangazwa na malalamiko hayo, kwa kuwa tayari wameishanunua sukari ya viwanda vyote hadi itakayozalishwa Machi mwakani.
Katika ununuzi huo, Dewji alisema hata pale walipohitaji zaidi, waliambiwa kuwa imekwisha na kutokana na kauli ya Mwenyekiti wa viwanda vya Sukari, Mark Bainbridge, aliyoitoa kwa waandishi waliofanya ziara kiwanda cha Kilombero, wapo tayari kununua sukari yote iliyobaki kwenye maghala yao.
Katika ziara ya waandishi iliyofanyika mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kujionea hali halisi ya mrundikano wa sukari uliotokana na uagizwaji bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi, kulibainika kuwepo kwa tani 158 zinazoozea kwenye ghala huku tani 40,000 zikishindwa kuuzika.


Pia katika sakata hilo, wakulima wa miwa wameonekana kukatishwa tamaa kuendelea na kilimo hicho, ambako kwa sasa wanadai bei imeshuka kutoka sh 69,000 kwa tani hadi kufika 55,000 jambo linalowafanya kufikiria kurudi katika kilimo cha mpunga walichokuwa wanakifanya awali.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji