Zitto, Filikunjombe wadai waziri alitaka kuiba ripoti
Dar es Salaam.
Viongozi wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na Deo Filikunjombe wamemtuhumu Waziri William Lukuvi kuwa alitaka kuiba ripoti ya kamati yao kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Sakata hilo lilihitimishwa Jumamosi wakati Bunge lilipoazimia kuwajibishwa kwa watu wote waliohusika kwenye uchotwaji wa fedha hizo, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa taasisi za fedha zilizoruhusu kufanyika kwa miamala mikubwa kinyume na taratibu za kibenki. Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili kutoka Chadema na CCM walilieleza gazeti hili kuwa jaribio hilo lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM) kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi ilipowasilishwa bungeni.
Hata hivyo, Lukuvi alikanusha vikali tuhuma hizo akisema kuwa aliipata ripoti hiyo siku iliposomwa na kwamba kama angehusika, asingekubaliwa kuwa mjumbe wa kamati ya maridhiano iliyoundwa mwishoni mwa kikao kupendekeza maazimio ya Bunge.
“Si kweli,” alisema waziri huyo wa nchi anayehusika na sera, utaratibu na Bunge.
“Unajua PAC walikuwa wanafanya kazi chini ya hazina. Hata Spika wa Bunge hakuiona hiyo ripoti, aliisikia tu ikisomwa bungeni. Kwanza kamati ilikuwa ikidurufu hiyo taarifa yake eneo la mbali na ili uipate ilikuwa ni lazima umrubuni Zitto.”
Aliongeza kusema: “Kama kweli nilikuwa nataka kuiba taarifa yao nisingekubali kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya maridhiano, iliyokutana kupitia upya mapendekezo ya PAC baada ya yale ya awali kuzua mvutano bungeni.”
Hata hivyo, Filikunjombe, ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa walilazimika kumwondoa eneo la kuchapishia ripoti hiyo. “Waziri Lukuvi alitumwa saa 9:00 usiku kuiba taarifa yetu wakati tunaichapa. Taarifa ilikuwa katika ‘flash’ na tulipogundua hilo tulimfukuza. Sisi tuliamua kuilinda ripoti ili isiibwe,” alisema Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM.
“Ile taarifa tuliichapa usiku wa kuamkia Jumatano ambayo ilikuwa siku ya kuiwasilisha bungeni. Na hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kikao cha Bunge kuahirishwa mara tu baada ya PAC kuwasilisha taarifa yake, ili Serikali ikajipange,” aliongeza.
Mbali na kauli yake ya jana, Filikunjombe aligusia suala hilo la ulinzi wakati akishukuru wabunge kwa kushikamana katika kufikia maazimio manane ya kuwawajibisha wote waliohusika.
Katika shukrani hizo, Filikunjombe alisema walilazimika kukesha usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kuilinda ripoti yao isiibiwe na hivyo kuwashukuru watendaji wa Bunge kwa kazi nzuri.
Hata hivyo, kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo kulienea taarifa kuna watu waliiiba na kunyofoa kurasa zilizokuwa na nyaraka za vielelezo na baadaye kuanza kuzisambaza. Polisi ilidai baadaye kuwa ilimkamata mtu aliyekuwa akisambaza vitabu hivyo vya ripoti, lakini hadi leo hajafikishwa mahakamani wala hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na polisi kuhusu maendeleo ya mtuhumiwa huyo.
Katika sakata hilo kubwa la aina yake, Bunge limtia hatiani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eliachim Maswi na wakurugenzi wa Shirika la Umeme kwa kuhusika kwa makusudi au kwa uzembe katika kufanikisha miamala haramu kutoka kwenye akaunti hiyo.
Habari hii ni kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni