Lwakatare wa Chadema, Ludovick waibwaga Serikali mahakamani

Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare 
 Mahakama ya Rufani imetupilia mbali maombi ya marejeo kuhusu uhalali wa uamuzi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam kuwafutia mashtaka ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezahura.
Hatua hiyo ya mahakama imefanya kiongozi huyo wa Chadema na mwenzake kuibwaga Serikali kwa mara ya pili mahakamani katika mashitaka dhidi yao.
Maombi hayo namba 5 ya mwaka 2014, yalifunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika Mahakama ya Rufani akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufumfutia mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Uamuzi wa kutupilia mbali maombi hayo ulisomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma kwa niaba ya Jopo la Majaji watatu wa mahakama hiyo lililokuwa limepangwa kusikiliza maombi hayo.
Majaji hao ni Nathalia Kimaro (kiongozi wa jopo), William Mandia na Profesa Ibrahimu Juma.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa maombi hayo yalikuwa na dosari za kisheria kutokana na DPP kutoambatanisha mwenendo wa uamuzi wa Mahakama Kuu aliokuwa akiupinga.
Dosari hiyo iliibuliwa na Jaji Prosefa Juma katika tarehe ambayo maombi hayo yalikuwa yamepangwa kusikilizwa ambapo alihoji iwapo ni halali kusikiliza maombi hayo bila kuwepo kwa mwenendo huo.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Angaza Mwipopo akisaidiana na Wakili Serikali Mwandamizi, Hashim Ngole, alijibu kuwa wanachopinga ni uamuzi wa mahakama kufuta mashtaka katika kesi ambayo haikuwa mbele yake.
Wakili Angaza alidai kwamba kutokuwepo kwa mwenendo huo hakuathiri na kwamba mahakama ina uwezo wa kuyasikiliza maombi hayo hata bila kuwepo kwa mwenendo huo.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Lwakatare, Peter Kibatala alisema kuwa suala la mwenendo wa uamuzi unaopingwa ni miongoni mwa hoja za pingamizi lake la awali dhidi ya maombi hayo.
Wakili Kibatala alidai kuwa kutokuwepo kwa mwenendo huo ni dosari ambayo ina athari kubwa kiasi kwamba mahakama haitakuwa na uwezo wa kutoa kile kinachoombwa.
Alisisitiza kuwa kutokuwepo kwa kumbukumbu za mwenendo huo ni athari ambayo tiba yake ni mahakama kuyatupilia mbali maombi hayo.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Wazazi timizeni wajibu wenu katika Malezi ili Watoto wenu wafikie Ndoto zao