Wapinzani walia CCM kuwachezea rafu
Dar es Salaam.
Vyama vya CUF na Chadema vimekitupia lawama Chama cha Mapinduzi (CCM) vikidai kimecheza rafu katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika leo.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti viongozi wa vyama hivyo walidai kuwa CCM imekuwa ikicheza mchezo mchafu kwa kuwarubuni na kuwanunua wagombea wake maeneo mbalimbali nchini.
Tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi huo mapema mwezi huu, CCM imekuwa ikitupiwa lawama za kuhujumu wapinzani na kwamba inatumia nafasi iliyonayo ya chama tawala kuvikandamiza vyama pinzani.
Hata hivyo, alipotafutwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ili kujibu shutuma hizo zilizotolewa na vyama vya Chadema na CUF alisema: “Siwezi kujibu chochote kwa sababu nyie ninapotoa majibu yangu hamuandiki ipasavyo lakini hao... Mnawaweka kipaumbele. Sasa basi andika walichosema halafu mimi kesho (leo) nitawajibu walichokisema kama kitakuwa na maana.”
Awali, huku akijigamba kuwa na asilimia 85 ya wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema: “Lakini yapo maeneo ambayo dakika za mwisho wagombea wetu ama kwa makusudi ama kwa bahati mbaya wakaingia mitini.”
“Asilimia nyingine zimekuja kupungua kwa hila na njama ambazo zimekuwa zikifanywa na CCM, zikiwamo kununua wagombea wetu, kuwateka, kuwanyanyasa kisaikilojia na maeneo mengine machache ni kutokana na mapingamizi yaliyowekwa ambayo hayakuwa na mantiki,” alieleza Mwalimu.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Mpango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alidai kuwa wana uthibisho wa kutosha kwamba CCM kwa kutumia mikono ya Serikali wamejiandaa kuvuruga zoezi la uchaguzi huo ili kupora ushindi, unaoelekea kwenye vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“CCM wameandaa karatasi za kupigia kura zenye alama ya vema kwa mgombea wao ambazo watawapa wananchi waiingie nazo kwenye chumba cha kupiga kura na kuwalipa kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000 kwa atakayefanikisha mpango huo,” alisema Mketo huku akiwaonyesha waandishi wa habari mfano wa karatasi hizo na kuongeza:
“Walianza mbinu hizi kwa kuwaengua wagombea wetu ili wa kwao wapite bila kupingwa katika maeneo ambayo Ukawa wana nguvu ila kwa hili la karatasi, tutapambana hadi mwisho.”
Akizungumzia juu ya mwitikio wa kujiandikisha katika zeozi la leo la kupiga kura, Mwalimu alisema kuwa Dar es Salaam imekuwa na mwitikio hafifu kulinganisha na mikoa mingine nchini.
“Mimi nashangaa sana, badala ya watu wa jiji hili kujitokeza kujiandikisha ili waweze kupiga kura na hatimaye wapate viongozi wanaowataka kushughulikia matatizo yao wao wanagoma…Ni asilimia 43 tu ya wakazi wa jiji hili waliojiandikisha kupiga kura leo,” alisema Mwalimu kwa masikitiko.
Alisema watu wengi hawana mwitikio kwa madai kuwa wanashughuli nyingi na wengine wakidai kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unawagusa watu wa vijijini ambako kuna matatizo mengi.
Maoni
Chapisha Maoni