JK akagua gwaride la mwisho la Uhuru
Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete jana alikagua gwaride la Uhuru la vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo baadaye vilipita mbele yake kutoa heshima ikiwa ni maadhimisho ya miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika.
Ikiwa hakutakuwa na mabadiliko yoyote, kiongozi huyo wa awamu ya nne wa Tanzania, anatazamiwa kustaafu kikatiba mwakani kabla ya sherehe nyingine za Uhuru Desemba 9, 2015.
Kwa kawaida uchaguzi mkuu hufanyika wikiendi ya mwisho ya Oktoba na matokeo hutangazwa siku chache baadaye. Kwa maana hiyo, hilo lilikuwa gwaride la mwisho la sherehe za Uhuru kwake akiwa mkuu wa nchi.
Mbali na hilo, wakati Rais Kikwete akifanya shughuli hiyo, macho ya Watanzania yalikuwa yameelekezwa kwake kuona jinsi anavyotekeleza jukumu hilo siku ya pili tu baada ya kutoka katika mapumziko ya upasuaji wa saratani ya tezi dume huko Marekani Novemba 8.
Kabla ya tukio hilo lililofanyika Uwanja wa Uhuru, juzi Rais Kikwete alionekana katika picha akifanya mazoezi mepesi siku 10 tu baada kurejea nchini akitokea Hospitali ya Johns Hopkins, Baltimore alikotibiwa.
Jana, Rais Kikwete alidhihirisha kuimarika kiafya baada ya kumudu kukagua gwaride hilo na baadaye mchana akasimama kwa muda mrefu akitoa nishani za heshima kwa watu mbalimbali waliolitumikia Taifa.Rais, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alitembea kwa mwendo wa ukakamavu akiwa ameongozana na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange kukagua gwaride hilo.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi walisikika wakimshukuru Mungu kwa jinsi alivyosaidia afya ya Rais kuimarika.
“Jamani kweli Rais Kikwete sasa yupo poa anatembea kwa mwendo wa ushupavu haswaa,” alisema mkazi wa Kinondoni Juma Ramadhani.
Rais Kikwete pia alisimama kwa muda mrefu kupokea salamu za kijeshi kutoka kwa gwaride hilo.
Sherehe zafana
Rais Kikwete aliingia kwenye Uwanja wa Uhuru saa 5.08 asubuhi akiwa katika gari la wazi huku akiwa ameambatana na Jenerali Mwamunyange.
Wakati akiingia, Kikwete alikuwa akitabasamu na kuwapungia mikono wananchi waliofika kwenye uwanja huo ambao walijibu kwa kumshangilia.
Maoni
Chapisha Maoni