Deni la Taifa linapotiliwa shaka

Limekuwa jambo la kawaida sasa kwa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za kila mwaka kuibua madudu mengi ya kutisha kuhusu matumizi ya fedha za Serikali. Moja ya mambo ya ajabu yanayoibuliwa na kuwashangaza wananchi wengi ni kukua kwa deni la Taifa kwa kasi ya kutisha, lakini Serikali ikionekana kutokuwa na uhakika kuhusu deni halisi la Taifa.
Uhakiki wa mchanganuo wa deni la Taifa kwa mwaka 2012 ulibaini kuwapo kwa marekebisho ya deni la Sh620 bilioni ambalo Serikali ilishindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa jumla, Ripoti ya CAG ilibainisha kwamba deni la Taifa linazidi kupaa. Mwaka huo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, deni hilo lilikua kwa asilimia 17 kulinganisha na mwaka uliotangulia. Hatuhitaji kupiga ramli kutambua kwamba kuna ufisadi wa kutisha katika Akaunti ya deni la Taifa. Kukosekana kwa maelezo ya kuridhisha kuhusu fedha hizo ni jambo lililopaswa kuibua maswali mengi.
Mwaka wa fedha uliopita deni la Taifa lilikuwa Sh22 trilioni na tunaambiwa sasa kwamba tayari limepaa hadi Sh30 trilioni mwaka huu. Tunajiuliza jinsi deni hilo linavyoweza kupaa kwa kasi hiyo ya kutisha katika muda mfupi. Utafiti uliofanywa Juni mwaka huu na Taasisi ya Muungano wa Madeni Tanzania (TCDD), umeonyesha kuwapo kwa shaka kuhusu deni hilo kutokana na kutokuwapo ofisi ya pamoja ya kusimamia deni hilo na kuwapo kwa maofisa wasiothibitishwa kuchukua mikopo bila idhini ya mamlaka husika.
Wizara ya Fedha imeonyesha udhaifu mkubwa katika kusimamia na kuratibu deni hilo kiasi cha kuwa na kigugumizi yanapokuja masuala ya kutambua kiwango halisi cha deni hilo na sababu zilizosababisha kukua kwa deni hilo kwa kiwango hicho cha kutisha. Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna mamlaka inayoweza kufanya mchanganuo wa matumizi yaliyosababisha kuwapo kwa deni hilo kubwa.
Mwaka jana wakati deni hilo lilipokuwa Sh22 trilioni, Sh2 trilioni hazikuweza kutolewa maelezo na Serikali, ambayo mpaka sasa haina mkakati unaoeleweka siyo tu wa jinsi ya kulipa deni hilo, bali pia kutambua kiasi ambacho nchi yetu inadaiwa. Wataalamu wa uchumi wanasema Serikali inaendelea kukopa kiasi kikubwa cha fedha kuliko kile inachokusanya kwa njia ya kodi na vyanzo vingine vya mapato. Kwamba inaendelea kukopa fedha kwa matumizi ya kawaida badala ya miradi ya maendeleo ambayo ndiyo inapaswa kuwa vipaumbele vya taifa.
Inahofiwa hivi sasa kwamba upo uwezekano wa kuwapo kwa deni kubwa zaidi ya Sh30 trilioni kutokana na utoaji wa taarifa kwa kutumia takwimu za kuokoteza. Inasemekana ipo mikopo ambayo haijatolewa taarifa na Msajili wa Hazina na mikopo hiyo ikihamishiwa kwa Serikali.
Mifano ya mikopo hiyo mikubwa ni mingi, ingawa Ripoti ya Utafiti wa TCDD ilipendekeza Serikali kutunga sheria ya kuanzisha ofisi ya pamoja ya kusimamia deni la Taifa na kuitaka Serikali kutekeleza mapendekezo ya CAG ya kufanya ukaguzi wa deni hilo, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu deni hilo kwa lengo la kuliweka wazi kwa wananchi. Kutokana na hali hiyo tata, tunadhani litakuwa jambo jema iwapo Serikali itawafahamisha wananchi kuhusu deni halisi la Taifa, kwani wao ndiyo wenye jukumu la kulilipa.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Matumizi ya simu kwa wanafunzi chanzo mmomonyoko wa maadili’

HATARI: Wengi wanunua sabuni za dawa bila maelekezo ya wataalamu

Kibondo;Chuo cha Uuguzi kilichoko Wilayani Kibondo mkoani Kigoma kina kabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ya majengo fedha kwa ajili ya kuendeshea chuo hicho na ukosefu wa watumishi wakutosha hali inayopelekea kuathili ufundishaji