Mganga achoma moto wateja
Kilindi.
Mganga wa tiba za asili, Omari Kikukwa (32) mkazi wa Kijiji cha Bondo , Kata ya Mswaki wilayani hapa anashikiliwa na polisi kwa kuwachoma moto wateja wake na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Aziza Hassani (35) mmoja wa mwanafamilia aliyenusurika kwenye mkasa huo akisimulia kuwa ilikuwa tarehe 27 mwezi uliopita yeye, mama yake pamoja na watoto wake wawili walipelekwa kwa mganga wa kienyeji na baba yao wa kufikia kwa ajili ya kufanyiwa tambiko.
Alisema kuwa walifika kwa mganga huyo na kuanza kufanyiwa dawa ambapo ilifanyika ndani ya shimo ambalo liliezekwa nyasi kavu juu yake na kuachwa nafasi ndogo kwa ajili ya kuingilia ndani ya shimo hilo waliloambiwa ndiko dawa inatakiwa kufanyika huku baba yao akibaki nje na mganga.
Anaeleza kuwa baada ya muda walidhani mganga ameshamaliza na kumuuliza wanaweza kutoka ila aliwajibu dawa bado inaendelea ambapo ghafla mganga huyo aliwasha moto juu ya zile nyasi na moto mkubwa ukaanza kuwaka ndipo akawaamrisha watoke shimoni huku moto ukiendelea kuenea hadi mlangoni.
Alisema ilibidi aanze kumrusha nje mwanaye mdogo Hassani Rajabu (4) halafu kuanza harakati kwa ajili ya kumsaidia mama yake na mwanaye Zuhura Rajabu ambapo hakufanikiwa kutokana na moto kuwa mkubwa hivyo yeye aliungua kichwani huku mama yake na mwanaye miili yao ikiwa imeungua vibaya.
Alisema baada ya moto kupungua walitoka huku wenzie wakiwa hawajiwezi kabisa ambapo baba yake na mganga walimkataza wasipeleke majeruhi hospitali ila kuna daktari wao anakwenda kuwatibu katika kijiji cha jirani na hapo.
Aziza alisema huko kwa huyo daktari hakuna kilichofanyika kwa siku tatu hadi kufikia Desemba mosi mama yake Hadija Abdallah(65) alifariki dunia hapo hapo kijijini huku hali ya mwanaye nayo ikizidi kuwa mbaya kutokana na kukosa tiba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraisser Kashai amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa amekamatwa na tayari ameshafikishwa mahakamani Desemba 8 mwezi huu kwa kosa la mauaji na kujeruhi kwa moto watu watatu.
Maoni
Chapisha Maoni